Kiswahili ya tukuka tamashani - Kenya

by Karare Jane Njeri
(Nairobi)


Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka uliopita uliwatia tumbo joto weledi wengi wa lugha ya Kiswahili. Kisa na maana ni kwamba lugha ya Kiswahili ilikuwa imerudi nyuma zaidi katika matokeo ikilinganishwa na matokeo ya miaka iliyopita.

Nyuso za wengi zilipata afueni mara walipoketi kutazama tamasha za michezo ya kuigiza iliyofanyika Nakuru katika chumba cha Lohana. Uumbuji wa hali ya juu ulidhihirika jukwaaani huku wanafunzi wakijizatiti kujipa uhusika mbalimbali ili mchezo uwe wa kufana.

Kilichopendeza zaidi ni kuona jinsi lugha ya Kiswahili ilivyopewa kipaumbele katika baadhi ya tungo zilizowasilishwa. Wanafunzi wa shule ya watoto ya Victorious walikariri ngonjera yenye mada Tunasema tunataka. Ujasiri na matumizi ya lugha fasaha ya Kiswahili huku ikiandamana na maudhui mbalimbali ya elimu iliwaaacha wengi vinywa wazi. Watoto walionekana kufahamu kile wanachohitaji maishani na nyota yao ya ufanisi waliiona kwa karibu mno na uhakika mwingi.

Wanafunzi wa Carol Academy walikariri ngonjera Eti nini Eti wapi? Iliyokuwa na malengo ya kuwazindua Wakenya kuhusu hasara ya uhasama kati yao na majirani zao. Mada kuu iliyojitokeza katika maonyesho haya ni haja ya kuwa na umoja wa nchi na masikizano.Shule ya upili ya Musikoma kutoka Bungoma ilichochea umahiri wa Kiswahili kupitia kwa ngonjera yao Cindelisa. Mbali na ngojera, shairi lao pia lilinyakua nafasi ya kwanza katika maonyesho haya. Kinachotia moyo ni kuona jinsi misamiati wa lugha ya Kiswahili ulivyotumiwa. Mtiririko na muwala wa sentensi katika kazi hizi ni wenye kuvutia na kupendeza masikioni pa msikilizaji.

Mbali na maonyesho katika lugha ya Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa pia zilipata nafasi zao ijapokuwa sio kwa kiasi kikubwa ililinganishwa na Kiswahili. Shule ya Nairobi school iliwazuzua watazamaji kwa mchezo wao Fourty minutes, uliotoa picha halisi ya mauaji ya kinyama yaliyotokea kanisani huko Kiambaa. Lengo kuu lilikuwa kuwahimiza Wakenya kuwa na undugu na kuishi kwa amani. Melchizedek ni mchezo ulioigizwa na wanafunzi kutoka shule ya Alliance. Ngoma za kitamaduni nazo hazikubaki nyuma. Shule ya Kakamega, ilinyakua nafasi ya kwanza kwa ngoma yao Sitela. Wanafunzi kutoka shule ya msingi ya Peace pia walisakata ngoma ya kitamaduni yenye mada Moraa. Mchezo wa kuigiza uliobeba kombe la siku katika kitengo cha shule za msingi uliwasilishwa na shule ya msingi ya Lions Nakuru. The letter, ni mchezo wa kuigiza unaomhusu msichana aliyelelewa na wazazi ambao hasa hawakuwa mama na baba yake. Baadaye, anakuja kugundua kwamba mamake alimtupa pipani na kutoweka akiwa mchanga.

Tamasha hizi ziliwavutia Wakenya wengi kutoka pembe zote za nchi hata ingawa tumekuwa na misukosuko na wasiwasi mwingi nchini. Walimu na wanafunzi walijizatiti na kutumia muda mdogo waliokuwa nao ili kutayarisha michezo mbalimbali na kufanikisha tamasha hizi. Wakenya tuna changamoto ya kuienzi lugha hii kama alivyosema mwandishi Shaaban Robert "Titi la mama litamu, lingine halishi hamu, Kiswahili lugha adhimu lazima tuienzi."
Na Njeri Karare
njeka84@yahoo.com

Click here to post comments

Join in and write your own page! It's easy to do. How? Simply click here to return to General Chat .